Moja kati ya Habari iliyofuatiliwa zaidi na kukamata headlines duniani ni pamoja na Rais wa zamani wa nchini Marekani Donald Trump kuwasili jijini New York mwanzoni mwa wiki hii ikiwa ni siku moja kabla ya kujisalimisha kwa mamlaka na kufikishwa mahakamani mnamo tarehe 4 April 2023 kwa mara ya kwanza kujibu mashtaka ya uhalifu.
Donald Trump aliondoka nyumbani kwake eneo la Mar-a-Lago jijini Palm Beach, katika jimbo la Florida akielekea kwenye uwanja wa ndege wa LaGuardia huku akisindikizwa na msafara wa takriban magari 11 aina ya SUV yenye rangi nyeusi na moja likiwa na rangi nyeupe ambalo inasekana ndio alilotumia mwenyewe, heka heka hizi zilikuwa katika harakati za kuelekea jijini New York kwa ajili ya kesi inayomkabili Rais huyo wa zamani. Trump alisafiri kwakutumia ndege yake ya “Trump Force One” ikiwa ni ndege ya kibinafsi aina ya Boeing 757 yenye thamani ya dola milioni 100 na hivi karibuni aliifanyia ukarabati baada ya miaka miwili ikiwa na chumba cha kulala na mikanda ya usalama iliyofunikwa kwa dhahabu. Ndege hiyo imetumiwa na Trump tangu 2011.
Trump alipotua alielekea kwenye makazi yake ya “Trump Tower” katikati mwa jiji la Manhattan kwaajili ya kupumzika. Trump ndie rais wa kwanza kushtakiwa kwa makosa ya jinai wiki iliyopita, wakati baraza kuu la mahakama la Manhattan lilipopiga kura kumshtaki kwa kosa lake la kulipa kumhonga Mwanamke ambae ni nyota wa filamu za ponografia aitwae Stormy Daniels ili aweze kuficha siri ya mahusiano waliyokuwa nayo kabla ya Uchaguzi wa mwaka 2016.