Leo May 30, 2018 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema viwango vya maambukizi ya UKIMWI nchini bado ni vikubwa na vinaongezeka katika baadhi ya mikoa.
Majaliwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 15 ya kuanzishwa kwa Mfuko wa dharura wa Rais wa Marekani kupambana na Ukimwi (PEPFAR) ambapo imetenga Trilioni 10.26 tangu ulipoanzishwa 2003.
Waziri Majaliwa amesema kuwa pamoja na mafanikio ya kupambana na UKIMWI bado kuna kazi kubwa mbele ya kupambana na ugonjwa huo.
“Utafiti wa nne uliofanyika katika ngazi ya kaya kuanzia October 2016 hadi August 2017 unaonyesha wastani wa kitaifa wa maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 4.7,” amesema Waziri Mkuu
Pia wanawake ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.1, pia watu Milioni 1.4 wanakadiriwa kuishi na VVU nchini.
Waziri Majaliwa amesema watu takribani 81,000 hupata maambukizi mapya ya VVU kila mwaka sawa na watu 222 kila siku na wengi wao ni vijana kati ya miaka 15 hadi 24, hususani wasichana.
Naye Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Inmi Patterson amesema serikali ya Marekani imewekeza Shilingi trilioni 10.26 tangu 2003 kudhibiti maambukizi ya UKIMWI nchini Tanzania.
“Ili kudhibiti janga hili, ni muhimu sana kwa Watanzania wote wanaoishi na VVU kupima na kujua hali za afya zao na kisha kuanza matibabu yatakayookoa maisha yao,” amesema.