Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA) imetia Saini mkataba na kampuni ya Indra Avitech GmbH wenye thamani ya shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya kubuni, kusambaza, kusanikisha, kuunganisha na kuzindua mfumo wa usimamizi wa taarifa za Anga (AIM).
Lengo la utekelezaji wa mradi wa mfumo huo ni kuboresha mfumo wa AIM katika kuboresha usahihi wa data, upatikanaji na ufanisi kwa kuzingatia mahitaji ya upandishaji wa mfumo wa Anga wa usafiri (ASBU) na kufuata viwango vya kitaifa na Kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa Habari Septemba 22 mwaka huu Jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji Saini mkataba, Mkurugenzi Mkuu Wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema mradi huo utatekelezwa kwa miezi 18 na utaanza mara tu baada ya kusainiwa kwa mkataba.
Alisema Tanzania inakuwa nchi ya Tano Afrika kufunga mfumo huo ikiwa ni baada ya nchi ya Kenya, Uganda, Eswatini na Ghana.
“Hii ni sehemu ya mpango thabiti wa AIM wa kuboresha mfumo wake wa taarifa za Anga kwa kutoa usimamizi wa taarifa za Anga kwa njia ya kisasa zaidi kwa kutoa na kubadilishana taarifa za Anga za kidigitali zenye ubora na kushirikiana na pande zote hivyo kuhakikisha usalama, utaratibu na ufanisi wa usambazaji wa anga wa kitaifa na kimataifa”
Aidha alisema kwa sasa TCAA imekuwa ikisimamia taarifa za Anga kwa jianya kawaida, NoTAMs kutengeneza nyaraka muhimu za AIM kama mchapishaji wa taarifa za Anga na kutoa huduma za Mipango ya safari na utambuzi wa awali wa safari hivyo kuimarisha michakato hiyo kwa njia ya kiotomatiki kutaimarisha uzingatiaji wa TCAA kwa viwango na taratibu zinazopendekezwa na shirika la usafiri wa anga la Kimataifa na kuleta manufaa kwa wadau kwa kuboresha utoaji wa huduma za AIM.
“Wadau wa TCCA wanapaswa kutarajia upatikanaji wa wakati unaofaa wa taarifa za Anga zenye ubora wa hali ya juu kwa muundo wa digitali, Mipango ya safari yenye ufanisi na huduma za utambuzi kupitia mfumo wa Mipango ya safari kwenye wavuti.
Makampuni ya ndege na watoa huduma za Anga wataweza kutekeleza huduma za utambuzi kabla ya safari katika eneo lao, watakuwa na upatikanaji wa taarifa zote muhimu kama NoTAMs, taarifa za hali ya hewa na taarifa za mchapishaji wa Taarifa za Anga wa elektroniki mtandaoni ili kupanga safari zao kwa ufanisi” Alisema Mkurugenzi Johari
Alisema watoa taarifa za Data wa TCAA wanapaswa kutarajia kuboresha njia wanayosambaza taarifa muhimu kwa idhini ya TCAA kwani tovuti ya kutoa Data itaruhusu watengenezaji wa Data za Anga kuwasilisha taarifa muhimu kwa TCAA badala ya kutumia mchakato wa kawaida wa kibinafsi.
Meneja Miradi na Mauzo kutoka kampuni ya Indra Avitech, Simon Masike alisema programu hiyo itawezesha data za anga kuhifadhiwa na kuhamishiwa kwenye programu maalumu kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za anga kwa njia ya kiotomatiki.
“Tunafurahi kuwa sehemu ya kutekeleza mradi huu ambao utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha usalama wa safari za angani kutokana na kutoa taarifa zenye ubora,” alisema Masike.