Manchester United inaweza kumkosa mlinda mlango Andre Onana kwa hadi mechi tisa baada ya kuisaidia Cameroon kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Onana alibatilisha kustaafu kwake kimataifa mwezi uliopita na aliichezea Cameroon mechi yake ya kwanza tangu mechi yao ya ufunguzi ya Kombe la Dunia dhidi ya Uswizi takriban miezi 10 iliyopita.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 awali alistaafu soka ya kimataifa baada ya kuzozana na meneja Rigobert Song kwenye michuano hiyo, lakini akarejea uwanjani katika ushindi wao wa 3-0 wa kufuzu AFCON dhidi ya Burundi.
Erik ten Hag huenda akalazimika kumgeukia mchezaji mwenzake mpya Altay Bayindir kuchukua nafasi ya Onana.
Wakati £47m zilitumika kumnunua Onana kama mbadala wa David de Gea, United walilipa £4.3m tu kumleta Bayindir Old Trafford kutoka Fenerbahce baada ya Dean Henderson kukamilisha uhamisho wa £15m kwenda Crystal Palace.