Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinatenga maeneo ya uwekezaji ili kurahisisha wawekezaji wanaokuja nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali bila usumbufu.
Dkt Mabula ametoa kauli hiyo tarehe 22 Februari 2023 wakati wa kikao kazi cha kujadili na kuweka mikakati ya kukwamua changamoto za sekta ya ardhi katika mkoa wa Morogoro kilichofanyika mkoani humo.
Waziri Mabula amesema, Mhe Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameifungua nchi kwa kukaribisha wawekezaji ambapo alieleza kuwa tayari wawekezaji wameanza kuja kwa wingi na kushindana kwenye sekta mbalimbali kama vile kilimo, viwanda , madini na ujenzi wa nyumba.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Rais Samia alielekeza kila halmashauri nchini kutenga maeneo ya uwekezaji hivyo ni jukumu la kila halmashauri kuhakikisha maeneo ya uwekezaji yanaandaliwa na kutengwa sambamba na kuwekewa mkakati utakaofanya maeneo hayo kuwa tayari kwa uwekezaji.