Kuibuka kwa ufa mkubwa katika eneo la Suswa katika Bonde la Ufa kusini magharibi mwa Kenya kumezua wasiwasi kuhusu uthabiti wa eneo la Afrika Mashariki kijiolojia. Wataalamu wanasema kutokea kwa ufa huo katika jimbo la Nakuru ni shughuli ya kijiolojia inayochukua muda mrefu ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda.
Hilo limezua hatari ya kuanza kutokea tena kwa mitetemeko ya ardhi na milipuko ya vilkano. Wanajiolojia wanasema baada ya mamilioni ya miaka, bara la Afrika litapasuka na kuwa vipande viwili.
Sehemu ya mpasuko itakuwa kwenye Bonde la Ufa jambo ambalo linazua uwezekano wa Kenya na Tanzania, pamoja na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, kujitenga na bara la Afrika.
Mwanajiolojia David Adede ameambia BBC kwamba ufa huo ni sehemu ya kutengana kwa vipande viwili vikubwa vya bara Afrika ambako kutasababisha bara Afrika kutengana na kuwa mabara mawili.
Amesema shughuli hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda lakini dalili zake zilikuwa zinafichwa na majivu ya volkano ambayo polepole yamekuwa yakiziba ufa kila unapotokea.
“Maji ya mvua yamesomba majivu hayo pamoja na mchanga na kuufanya ufa huo kuonekana zaidi,” David Adede
Anasema vipande hivyo vimekuwa vikitengana “katika kasi ya sentimita mbili kila mwaka.”
Kipande kilicho na sehemu kubwa ya bara hufahamika kama Kipande cha Nubia na kipande cha pili hufahamika kama Kipande cha Somalia.
Dkt James Hammond kutoka kwa Idara ya Sayansi na Uhandisi wa Dunia kutoka chuo cha Imperial College London alinukuliwa na jarida la mtandaoni la Mail & Guardian akisema: “Katika miaka milioni kadha ijayo, shughuli hii itakamilika na kuigawa Afrika mara mbili, na kuunda bahari mpya hapo katikati na bara jingine. Ukitumia jiografia ya sasa, bara hilo jipya litashirikisha Somalia, nusu ya Ethiopia, Kenya na Tanzania.”
Baadhi ya wanajiolojia wanakadiria kwamba huenda mpasuko huu ukayabeba pia mataifa ya Uganda, Rwanda, Burundi na maeneo ya Malawi na Msumbiji.
Via BBC