Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 59 yenye thamani ya shilingi trilioni 2 kuanzia mwezi Aprili hadi Mei mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Profesa Godius Kahyarara amezungumza na Baraza la Wafanyakazi wa TIC na kuwapongeza kwa kazi wanazozifanya kwani usajili wa miradi umeongezeka na ajira takribani elfu kumi na mbili (12).
Katika uzinduzi huo Prof. Kahyarara amewataka wafanyakazi kutekeleza mpango wa kanda maalum za kiuchumi lengo likiwa ni kurahisisha kuwahudumia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zao.
“Suala la Uwekezaji katika Kanda hizi za kiuchumi matarajio ya serikali ni tofauti na tulivyokuwa tunaona kwani ni muhimu sana kutekeleza maono ya namna hiyo. Ni jambo ambalo hatukutegemea Tanzania kuweza kuvutia wawekezaji na kupatikana kiasi cha shilingi trilioni 2 ndani ya miezi miwili (2) hivyo kwa muktadha huo kwa mwaka mmoja itakuwa trilioni ishirini na nne (24)” Prof. Kahyarara.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa miongoni mwa miradi iliyosajiliwa kwa kipindi hicho cha miezi miwili ya Aprili na Mei ni pamoja na sekta ya uvuvi na madini.
“Kumekuwa na ushirikiano wa karibu sana kati ya menejimenti ya TIC pamoja na wafanyakazi hivyo tumeona ufanisi umeongezeka kwa kasi sana, na miradi mingine iliyosajiliwa ni pamoja na kilimo na tehama” Dkt. Maduhu.
Aidha, Serikali imeanza kuboresha Uwekezaji kwakuwa imeanza mchakato wa kuwa na benki ya ardhi kwa kuunda timu inayohusisha Wizara ya Ardhi, Wizara ya Uwekezaji, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na TAMISEMI.