Mdhibiti wa taarifa na data muhimu nchini Uingereza ameitoza kampuni ya TikTok faini ya pauni milioni 12.7 (dola milioni 15.9) kwa ukiukaji kadhaa wa sheria ya ulinzi wa taarifa,pamoja na kutumia vibaya data ya kibinafsi za watoto wa nchini humo.
Ofisi ya Kamishna wa Habari (ICO) inakadiria kuwa mnamo 2020 TikTok iliruhusu zaidi ya watoto milioni 1 wa nchini Uingereza walio chini ya miaka 13 kutumia jukwaa hilo kwa kukiuka sheria zake. ICO ilisema hii leo kuwa TikTok haikufanya vya kutosha kuangalia ni nani anayetumia jukwaa lake na imeshindwa kuchukua hatua ya kuwaondoa watoto wenye umri mdogo na haikutoa taarifa sahihi kwa watumiaji kuhusu jinsi taarifa zao zilivyokuwa zikikusanywa na kutumiwa. Faini hiyo imetolewa kwa kosa la ukiukaji wa kanuni kati ya Mei 2018 na Julai 2020. John Edwards, Kamishna wa Habari wa nchini Uingereza alisema kuwa kuna sheria zinazotumika kuhakikisha watoto wako salama katika ulimwengu wa kidijitali kama walivyo katika ulimwengu halisia lakini TikTok haikufuata sheria hizo aliongeza kwakusema TikTok inapaswa kujua na kufanya maamuzi sahihi.
Msemaji wa TikTok aliiambia CNN kwamba kampuni hiyo imechukua hatua nyingi ili kudhibiti matumizi ya jukwaa hilo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 13 na kwamba haikubaliani na uamuzi wa ICO.
Serikali ya Australia inategemea kupiga marufuku matumizi ya TikTok kwenye vifaa vya serikali mwanasheria mkuu wa nchi hiyo alitangaza mapema hii leo, akielezea wasiwasi wake juu ya usalama huku Marekani, Uingereza na Canada zikiwa zote zimetangaza kupiga marufuku matumizi ya application hiyo kwenye vifaa vya serikali na pia Tiktok ilitakiwa kuondolewa kutoka kwenye vifaa vyote vilivyokuwa na uwezo wa kufikia taarifa za Bunge la New Zealand mwishoni mwa mwezi Machi, 2023