Mshawishi maarufu wa mitandao ya kijamii nchini Angola, Ana da Silva Miguel, anayejulikana kama Neth Nahara, ameshuhudia kifungo chake gerezani kikiongezwa hadi miaka miwili kwa “kumtusi” Rais João Lourenço kwenye TikTok.
Awali alihukumiwa kifungo cha miezi sita mwezi Agosti, mahakama ya rufaa iliamua hukumu ya awali ilikuwa ndogo na ikaongeza hadi miaka miwili.
Ana alimshutumu rais kwenye akaunti yake ya TikTok kwa “machafuko na ukosefu wa mpangilio,” na akamlaumu kwa masuala kama vile ukosefu wa shule, nyumba na ajira nchini.
Rais Lourenço alichaguliwa tena kwa muhula wa pili Agosti iliyopita, kuendeleza utawala wa muda mrefu wa chama cha MPLA. Chama hicho kimekuwa madarakani tangu uhuru wa Angola mwaka 1975 na kimekabiliwa na shutuma za kuongoza utawala kandamizi.
Mahakama ya rufaa katika mji mkuu, Luanda, ilitaja maneno ya kuudhi ya Miguel dhidi ya rais na ushawishi wake mkubwa kwa maoni ya umma kuwa sababu za hukumu hiyo kali zaidi.
Licha ya ombi lake la kuhurumiwa kama mkosaji wa mara ya kwanza na mama wa watoto wadogo ambaye alijutia matamshi yake, mahakama ilitupilia mbali ombi lake na kumwamuru amlipe Rais Lourenço $1,200 (£1,000) kwa “kuharibu” sifa yake.
Miguel, mwenye zaidi ya wafuasi 230,000 wa TikTok na maelfu ya maoni kwenye video zake, ndiye mtu wa kwanza nchini Angola kuhukumiwa kwa maudhui yaliyochapishwa kwenye TikTok, kulingana na wakili wake.
Uamuzi huo ni wa mwisho, kwani rufaa kwa Mahakama ya Juu inaruhusiwa tu kwa hukumu zinazozidi miaka mitatu.