Wananchi mkoani Tanga wametakiwa kutoa taarifa za wafanyabiashara wanaokwepa kutoa risiti pindi wanapofanya manunuzi Ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Tanga,ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanal Maulid Surumbu wakati wa maadhimisho ya siku ya mlipa kodi yaliyokwenda sambamba na kuwatambua walipakodi mahiri.
Amesema kuwa mkoa huo bado unachangamoto ya wafanyabiashara kutotoa risiti au kutoa risiti pungufu na malipo ya bidhaa iliyouzwa jambo ambalo linachangia kuikosesha mapato serikali.
“Wananchi niwaombe mkemee na kutoa taarifa za wafanyabiashara wasiotoa risiti Ili tuweze kuchukuwa hatua kwa wale wachache wasio na weledi”amesema DC Surumbu.
Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Tanga Thomas Masese amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 walipewa makadirio ya kukusanya Kodi ya sh Bil 233 lakini walikusanya sh Bil 214.3 sawa na asilimia 92.
Aidha katika udhibiti wa upotevu wa mapato ya serikali wameweza kufanya doria ya bidhaa za magendo na kukamata Mali zenye thamani ya sh Bil 2.5 .