Togo imechelewesha uchaguzi wa bunge na kikanda huku kukiwa na mvutano kufuatia mageuzi ya katiba yenye utata.
Mageuzi hayo yaliyoidhinishwa na wabunge wiki jana yalibadilisha mfumo wa urais na kuwa wa bunge.
Pia inakabidhi madaraka ya utendaji kwa waziri mkuu, na kupunguza mamlaka ya urais.
Vyama vya upinzani vimekataa mageuzi hayo, kwa kuhofia kuwa yanaweza kumwachia Rais Faure Gnassingbé kusalia madarakani.
Alimrithi babake, Gnassingbé Eyadéma, aliyefariki mwaka 2005 baada ya kutawala nchi hiyo kwa miaka 38.
Ofisi ya rais ilitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo siku ya Jumatano, lakini haikutoa tarehe mpya ya uchaguzi huo, ambao awali ulipaswa kufanywa tarehe 20 Aprili.
Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki wa Togo limemtaka Rais Gnassingbé kutotia saini mabadiliko ya katiba kuwa sheria, likitaja haja ya mashauriano mapana na mjadala wa kitaifa unaojumuisha mengi zaidi.