Wachezaji wa kimataifa wa Italia Sandro Tonali na Nicolo Zaniolo waliondoka katika makao makuu ya Azzuri siku ya Alhamisi baada ya kuambiwa walihusika katika uchunguzi wa waendesha mashtaka, Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) lilisema Alhamisi.
Wachezaji hao waliarifiwa kuhusu uchunguzi huo na waendesha mashtaka wa Turin wakiwa katika kituo cha mazoezi cha timu ya taifa huko Coverciano, kabla ya mechi za kufuzu kwa Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Malta na Uingereza.
FIGC haikubainisha uchunguzi huo ulihusu nini lakini ilisema viungo hao wawili waliruhusiwa kwenda nyumbani kwani shirikisho hilo liliamini kuwa hawakuwa katika hali nzuri ya kukabiliana na mechi zijazo.
Waendesha mashtaka wa Turin walisema Jumatano wanamchunguza mwanasoka mwingine wa Italia, Nicolo Fagioli, kwa madai ya shughuli haramu za kamari.
Fagioli anakabiliwa na uchunguzi sambamba na waendesha mashtaka wa FIGC ili kubaini ikiwa madai yake ya kamari yalihusisha michezo ya kandanda.
Mchezaji atakayepatikana ameweka kamari kwenye mechi za soka anaweza kufungiwa kwa angalau miaka mitatu na kutozwa faini ya angalau euro 25,000 ($26,520) chini ya kanuni za maadili za FIGC.
Tonali na Zaniolo wote wanacheza Ligi Kuu ya England.
Tonali mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na Newcastle United kutoka AC Milan mwezi Julai, wakati Aston Villa ilimsajili Zaniolo, 24, kwa mkopo kutoka Galatasaray ya Uturuki mwezi Agosti.