Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imefanya ziara maalum ya kutembelea na kutoa zawadi kwa walipa kodi wanaotekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari. Lengo kuu la ziara hiyo ni kuhamasisha wafanyabiashara wengine kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya taifa.
Ziara hiyo ilihusisha kutembelea maeneo mbalimbali ya biashara, ambapo TRA imewahimiza wafanyabiashara wasibweteke na pongezi walizopewa bali waendelee kuongeza juhudi katika ulipaji kodi, kwa lengo la kufanikisha maendeleo endelevu ya nchi.
Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Thomas Masese, alieleza kuwa mwaka 2024 umeanza kwa mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato, ambapo kuanzia Julai hadi Novemba, wamevuka matarajio ya ukusanyaji ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023.
Baadhi ya walipa kodi walioshiriki akiwemo Bw.Zarhan Lwahil wa kiwanda Cha kutengeneza Kadi za kielektroniki ameeleza kuwa ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka kwa viongozi wa TRA umewawezesha kuendesha biashara zao kwa ufanisi. Aidha, wameitaka mamlaka hiyo kuendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha biashara zao zinaendelea kuleta tija kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi nzima.