Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imeadhimisha Siku ya Shukrani kwa Mlipa Kodi kwa kufanya matembezi na kutoa misaada kwa makundi maalum, yakiwemo makazi ya wazee wa Mwanzange na vituo vya kulelea watoto yatima.
Katika shughuli hiyo, TRA ilitembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Goodwill Foundation na kuwapatia misaada mbalimbali. Aidha, mamlaka hiyo ilitoa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tanga Technical kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuwasaidia wanafunzi wa kike kuhudhuria masomo bila changamoto.
Akizungumza baada ya matembezi hayo, Kamishna wa Upelelezi wa Kodi TRA, Hashim Ngoda, aliwahimiza wafanyabiashara wote kuhakikisha wanajitokeza kufanya makadirio ya kodi zao kabla ya tarehe 31 Machi 2025 ili kuepuka adhabu kwa kuchelewesha makadirio hayo.
Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa kwa TRA kushirikiana na jamii, kuwashukuru walipa kodi kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa, na kuhamasisha utii wa hiari katika ulipaji wa kodi.