Shirika la Reli Tanzania – TRC yashirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA kukuza utalii wa ndani baada ya kutembelea kituo cha stesheni ya Mvave iliyopo karibu na mbuga ya Saadani Mkoa wa Pwani.
Stesheni ya Mvave ambayo iko mbioni kufungiliwa mara baada ya kukamilika kufanyiwa ukarabati na italeta hamasa kwa wananchi pamoja na wageni wanaotumia usafiri wa reli kwenda kutalii katika mbuga ya Saadani.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara TRC Bw. Never Diamond ameeleza kuwa ushirikiano baina ya TRC na TANAPA ni kuangalia miundombinu wezeshi ya kibiashara kati yao kujua jinsi ya kukuza utalii wa ndani kupitia usafiri wa treni.
“Treni ni usafiri mwepesi sana kwa abiria unaotumia gharama nafuu pia treni ni zaidi ya safari “ alisema Bw. Diamond.
Pia Bw. Diamond alisema kuwa stesheni ya Mvave ni stesheni muhimu katika kukuza utalii hivyo TRC na TANAPA imeweka mikakati mbalimbali ambayo itawezesha wananchi watumie muda wao kwenda kupumzika na kuona vivutio vilivyopo nchini.
“TRC tunaunga juhudi za Raisi wetu Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii wa ndani (Royal Tour)” alisema Bw. Diamond.
Naye Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi, kutoka katika Hifadhi ya Taifa Saadani Bw. Ephraim Mbomo amesema kuwa kituo cha Mvave kitabadilisha uwezo wa kupokea wageni wanaotumia magari ya kukodisha na kupata huduma ya moja kwa moja kwa kutumia usafiri wa treni.
“Treni ni usafiri wa uhakika katika vipindi vyote masika na kiangazi sababu wakati wa masika magari hupata shida kutokana na miundombinu ya barabara“ alisema Bw. Mbomo.
Aidha, Bw. Mbomo alieleza kuwa kwa mwaka hupokea wageni kwa wastani wa watu elfu 20 hivyo kupitia usafiri wa treni idadi ya wageni itaongezeka.
“Tumejipanga kuwapokea wageni watakaoongezeka , tayari tuna eneo la ‘dining’ lenye uwezo wa kuhudumia watu 300 pamoja na eneo la kambi ili tuweke mahema ya kutosha” alisema Bw. Mbomo.
Vilevile Bw. Mbomo alitoa shukrani kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia uzinduzi wa Royal Tour ambapo umeleta ongezeko kubwa la watalii kuja kuona vivutio mbalimbali nchini.