Rais wa Marekani Donald Trump ameonekana kubadili msimamo wake kuhusiana na uvaaji wa barakoa na kuwataka Wamarekani wavae barakoa wanapokuwa katika mikusanyiko ya watu ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.
Katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari baada ya miezi, Trump amesema hali ya virusi hivyo Marekani itakuwa mbaya kabla haijatengemaa, hii ni mara ya kwanza kabisa Trump kukiri kuhusiana na hali ilivyo mbaya nchini Marekani.
Rais huyo ambaye alikuwa akivipuuza virusi hivyo katika hatua zake za awali na kutaka kufunguliwa kwa uchumi wa nchi hiyo katika miezi ya hivi karibuni licha ya ongezeko la maambukizi, amekuwa hataki kuvaa barakoa mwenyewe.
Uvaaji wa barakoa Marekani umekuwa mjadala mkubwa huku baadhi ya wafuasi wa Trump wakisema kulazimishwa kuvaa barakoa ni kukiukwa kwa haki zao.