Mahakama ya juu zaidi ya Marekani imekataa jaribio la kubatilisha matokeo ya uchaguzi katika majimbo manne yenye ushindani mkubwa ambayo yalimuunga mkono Rais mteule Joe Biden.
Mashitaka, yaliyowasilishwa wiki hii na jimbo la Texas, yalilenga kubatilisha matokeo ya uchaguzi katika majimbo ya Georgia, Michigan, Pennsylvania na Wisconsin.
Rais mteule Biden alipata ushindi katika majimbo yote manne.
Mashtaka hayo yaliungwa mkono na Wanasheria wakuu wa majimbo 18 nchini Marekani na wajumbe wa Congress 106 kutoka Chama cha Republican.
Lakini katika maelezo mafupi ya kukataa azama hiyo, Mahakama kuu iliamua kuwa Texas haina haki ya kisheria ya kuleta kesi mbele ya mahakama hiyo.
Hukumu hiyo ni pigo kwa Trump , ambaye awali alisema bila ushahidi kwamba matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba yatatatuliwa na Mahakama ya ngazi ya juu .
Mahakama pia ilikataa mashitaka mengine ya kisheria dhidi ya ushindi wa Biden katika jimbo la Pennslvania mapema wiki hii, na kuyatupilia mbali madai hayo katika hukumu moja.