Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya utendaji ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa uchunguzi “usio na msingi” unaolenga Marekani na mshirika wake wa karibu Israel, Ikulu ya White House ilisema.
Agizo la Trump lilisema mahakama ya The Hague “imetumia vibaya mamlaka yake” kwa kutoa hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye alifanya mazungumzo na rais wa Marekani siku ya Jumanne.
Amri hiyo pia ilisema mahakama hiyo ilijihusisha na “vitendo visivyo halali na visivyo na msingi vinavyolenga Marekani na mshirika wetu wa karibu Israel,” ikimaanisha uchunguzi wa ICC kuhusu uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan na wanajeshi wa Israel huko Gaza.
Rais wa Marekani aliamuru kuzuiwa kwa mali na marufuku ya kusafiri dhidi ya maafisa wa ICC, wafanyikazi na wanafamilia wao, pamoja na yeyote anayeonekana kusaidia uchunguzi wa mahakama hiyo.
Vikwazo hivyo ni ishara ya uungwaji mkono baada ya ziara ya Netanyahu katika Ikulu ya White House, ambapo Trump alifichua mpango wa Marekani kuikalia na “kuchukua” Gaza na kuwasafisha kikabila Wapalestina katika nchi nyingine za Mashariki ya Kati.