Rais mteule wa Marekani Donald Trump, ameripotiwa kumwalika Rais wa China, Xi Jinping kushiriki katika sherehe ya kuapishwa kwake itakayofanyika Januari 20, 2025 licha ya ahadi yake ya kuweka ushuru mkubwa dhidi ya China ambaoi hatua hii imeelezwa kuwa ya kipekee kwani Marekani haina desturi ya kuwaalika Viongozi wa kigeni kwenye sherehe za kuapishwa kwa Marais wake.
Inaelezwa kuwa mwaliko huo ulitolewa mapema Novemba mara baada ya Trump kushinda uchaguzi ingawa bado haijathibitishwa ikiwa Xi atakubali mwaliko huo, tangu mwaka 1874 kumbukumbu rasmi zinaonyesha kuwa hakuna Kiongozi wa kigeni aliyewahi kuhudhuria sherehe kama hiyo ambazo kwa kawaida huhudhuriwa na Mabalozi na Wanadiplomasia wengine.
Timu ya Rais mteule Trump pia imeshusha wazo la kuwaalika Viongozi wengine wa Dunia kwenye sherehe hiyo na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, ambaye ni mshirika wa karibu wa Trump pia anafikiria kuhudhuria baada ya kumtembelea Trump wiki hii huko Mar-a-Lago.
Kwa upande wa uhusiano wa Marekani na China mvutano umeendelea kuwa mkubwa ambaoi Trump ametoa vitisho vya kuweka ushuru wa asilimia 100 kwa nchi za BRICS ikiwemo China iwapo zitajaribu kuanzisha sarafu mbadala ya Dola ya Marekani huku akiiwekea kampuni ya ByteDance inayomiliki TikTok, tarehe ya mwisho ya Januari 19, ili kuuza programu hiyo la sivyo ikabiliwe na marufuku Nchini Marekani.
Pamoja na hayo, Trump ameonyesha imani yake katika mahusiano ya moja kwa moja kati ya Viongozi wa Mataifa na katika mahojiano ya hivi karibuni,l alieleza kuwa alipata nafasi ya kuzungumza na Xi Jinping na walielewana vyema akisisitiza kuwa uhusiano wa karibu kati ya Viongozi ni muhimu kwa maelewano ya kimataifa.