Habari ya Asubuhi…!Karibu kwenye matangazo yetu hii leo Jumatatu 7.8.2023
Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, amesema atawasilisha pingamizi mahakamani, kutaka kesi dhidi yake kuhamishwa kutoka Washington pamoja na jaji anayesikiliza kesi hiyo aondolewe kwa kile anadai haoni kama atatendewa haki.
Trump ambaye amenusurika kwa zaidi ya mara mbili kuondolewa madarakani wakati akiwa rais, ambapo huenda akagombea kupitia Republican katika uchaguzi wa mwakani, amezidisha mashambulio dhidi ya waendesha mashtaka wanaosimamia kesi yake kuhusu kujaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Katika taarifa yake, Trump, amemtuhumu jaji Tanya Chutkan, akisema haamini ikiwa atamtendea haki katika kesi yake, akisisitiza anataka aondolewe au kesi hiyo kuhamishiwa jimbo jingine.
Haya hivyo wakili wake John Lauro, amekanusha madai ya Trump kupitia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa X, akisema bado uamuzi wa mwisho kuhusu hilo haujafanyika na kwamba wanafanya mapitio kabla ya kuamua.
Hatua ya Trump, inakuja baada ya jaji Tanya kutupilia mbali maombi ya mawakili wake kutaka kupewa muda zaidi kujibu hoja za mashtaka, ambapo wanatakiwa kuwasilisha majibu yao baadae hivi leo.
Ni jaji Tanya ambaye mwaka 2021, aliamua kesi dhidi ya Trump ambapo alisema rais sio Mfalme.