Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alithibitisha Jumapili kwamba hatashiriki mdahalo wa kwanza wa urais wa Jumatano wa chama chake cha Republican.
“Wamarekani wanajua mimi ni nani na kwamba urais wangu ulikuwa na mafanikio,” Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii, Truth Social. “Kwa hivyo sitafanya midahalo!” aliongeza.
Msemaji wake hakufafanua mara moja ikiwa anapanga kususia kila mdahalo au tu ule ambao umepangwa kwa sasa.
Rais huyo wa zamani na ambaye kura za maoni zinaonyesha kwamba anaongoza kati ya wale wanaowania tikiti ya chama cha Republikan ili kugombea urais, alikuwa amesema kwa miezi kadhaa kwamba hakuona haja ya kushiriki mdahalo huo wa kwanza msimu huu na wapinzani wake wa chama cha Republican ambao utafanyika mjini Milwaukee, jimbo la Wisconsin, siku ya Jumatano wiki hii, kutokana na kwamba anaongoza katika kinyang’anyiro hicho.
Mwanasiasa huyo pia alikuwa amewaeleza wazi wale aliozungumza nao siku za hivi karibuni kwamba maoni yake hayajabadilika.
Trump mara kwa mara amekosoa shirika la habari la Fox News, ambalo ndilo litaendesha na kupeperusha mdahalo huo, akisisitiza kuwa ni “ni lenye uadui” na anaamini halitamtendea haki.