Benki ya Letshego Faidika imetumia jumla ya Sh bilioni 5.3 kukopesha wateja 1,305 wa mkoa wa Mbeya.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Letshego Faidika, Adam Mayingu wakati wa ufunguzi wa taji jipya la benki hiyo maeneo ya Soweto mkoani Mbeya.
Mayingu amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kimekopeshwa kwa wateja wao mbalimbali serikalini na sekta binafsi.
Amesema kuwa Benki ya Letshego Faidika ni matokeo ya muungano kati ya taasisi ndogo ya kifedha, Faidika, na Benki ya Letshego Tanzania ambayo ilianza kufanya kazi Julai Mosi mwaka jana.
Mayingu amesema kuwa tawi la Mbeya lina historia ya kipekee ambapo kwa upande wa Benki ya Letshego ilianza kutoa huduma mwaka 2016 na kwa upande wa Faidika ulianza kutoa huduma mwaka 2008.
Amesema kuwa mpaka sasa wame kuhudumia wateja zaidi ya 3,417 kwa Mkoa wa Mbeya pekee. Pia, tuna satellite 6 ambazo ziko Ileje, Mkwajuni, Mbarali, Tukuyu, Kyela, na Mbozi.
Kwa upande wake,mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa aliipongeza benki hiyo kwa kufungua tawi hilo huku akiiomba kuongeza matawi zaidi mkoani humo na mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Malisa alisema kuwa Mbeya ni mlango wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ni fursa kwa benki hiyo kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika mikoa ya kusini.
Alisema kuwa asilimia 95 ya wakazi wa mkoa wa Mbeya ni wafanyabiashara ambapo endapo benki ya Letshego Faidika ikiwatumia vizuri, watapata faida kubwa.
Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Bw. Beno Malisa akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo mkoani Mbeya maeneo ya Soweto.