Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeombwa kutumia nguvu katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli’ na wenzake watano kwa sababu shauri hilo lipo tangu mwaka 2016.
Yusuf na wenzake watano, wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh.Mil 785.6.
Maombi hayo yametolewa na upande wa utetezi baada ya Wakili wa Serikali, Candid Nasua mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amedai kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilka.
Wakili wa Utetezi Neemia Nnkoko amedai rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2017 kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wameshangazwa kusikia upande wa mashtaka kuwa upelelezi bado haujakamilika ambapo wanaiomba mahakama itumie nguvu.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Simba alisema rekodi zinaonyesha kuwa Oktoba 23,2018 upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilka hivyo anawataka upande wa mashtaka wamueleze wakili wa Serikali. Mkuu Mchimbi kuhusu kukamilisha kwa upelelezi huo.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, 2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yao hayana dhamana.