Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imewaonya wananchi kutojiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za Uchaguzi.
Onyo hilo limetolewa leo na mkurugenzi wa Kitengo cha huduma za sheria Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mtibora Selemani kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacob Mwambegele kwenye mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika mkoani Njombe.
Amesema kujiandikisha mara mbili kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ni kosa la jinai kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi Rais,Wabunge na Madiwani Na.1 ya mwaka 2024.
“Kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu yeyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha laki moja (100,000) na isiyozidi laki tatu (300,000) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja” amesema Selemani.
Amesema zoezi hilo la uboreshaji wa Daftari haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo na ambao kadi zao hazijaharibika au kupotea au hawajahama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine au taarifa zao hazijakosewa au hawahitaji kuboresha taarifa zao.
Amewataka Mawakala na viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia sheria kwa kutoingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kwenye vituo.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi Stephen Elisante amesema kwa mkoa wa Njombe jumla ya wananchi 80994 wanatarajiwa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga kura.
“Vijana wawahamasishe wenzao kwa wingi na kujiepusha na upotoshaji kuhusu zoezi hilo muhimu” amesema Elisante.
Katibu wa Mafunzo Siasa na Uenezi kutoka Chama cha Mapinduzi mkoa wa Njombe Josaya Luoga amesema watafanya jitihada kuhakikisha wanawahamasisha wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari hilo.
“Sisi kama Chama cha Mapinduzi tunawahasa viongozi wetu na wanachama wetu kutoingilia michakato ya tume ya uchaguzi kwasababu tume ipo kisheria” amesema Luoga.
Naye katibu Uenezi wa Chama cha ACT Wazalendo Ally Mhagama amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha wakati wakiendelea kuufuatilia mambo mengine ambayo yamekuwa yakiharibu chaguzi.
“Tumeona baadhi ya vitu vinalalamikiwa vimetekelezwa wajitokeze kwenye mkoa wetu wa Njombe kujiandikisha maeneo yote huku tukiendelea kuangalia mifumo mingine ambayo haijakaa vizuri tukihakikisha inakaa vizuri” amesema Mhagama.