Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus ameelezea mafanikio ya ziara ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini India, wakati akiongea na Waandishi wa Habari leo Ikulu Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine amesema katika ziara hiyo, Tanzania imefanikiwa kupata uhakika wa soko la mbaazi na Rais Samia ameomba kupatiwa soko la mgawo wa uhakika wa tani laki mbili kwakuwa India ni Mtumiaji mkubwa wa mbaazi duniani.
“Nchi ambazo zimepata fursa ya mgao kama huo ni Malawi na Msumbiji kutoka India, hivyo sisi ni watatu kutoka Afrika, katika hatua nyingine Serikali ya Tanzania imewasilisha mahitaji kwenye Serikali ya India, kwa ajili ya mradi mkubwa wa umwagiliaji kutoka Ziwa Victoria, mahitaji hayo ni takriban dola Bilioni moja ambao mradi huo utatekelezwa mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Dodoma, Kagera na Mara”
“Pia Serikali ya Tanzania ina mpango wa kununua jumla ya trekta elfu 10 na kujenga vituo maalum vya vifaa vya kilimo (mechanization), Serikali imekubaliana na makampuni makubwa mawili duniani ya matrekta, Mahindra na John Deer kuweka katika kipindi cha miezi 12 viwanda vya kuunganisha matrekta na kutengeneza vipuri ndani ya Tanzania”
“Tukizungumzia Sekta ya Ulinzi, Nchi hizi mbili zinatambua umuhimu wa kushirikiana kwenye teknolojia (technology transfer), kujengeana uwezo, mafunzo ya jeshi kwa pamoja na kubadilishana utaalamu na uzoefu”