Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene, amesema kuwa wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi watajadiliana na kuangalia namna nzuri ya kuweza kuwapatia viwanja askari polisi ili kuwaepusha na fedheha wale wanaostaafu na kujikuta hawana kiwanja wala nyumba.
Kauli hiyo ameitoa Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Agnesta Lambert, lililohoji umuhimu wa serikali kuweka utaratibu wa askari polisi kusamehewa kodi ya vifaa vya ujenzi na kupewa viwanja kwa bei elekezi ili kuwaepusha na njia za udanganyifu kwa kigezo cha kwamba wanajiandaa na maisha baada ya kustaafu.
“Askari polisi wanafanya kazi nzuri kwa taifa lao na pengine wanafanya hivyo katika mazingira magumu na wengine kulingana na vyeo vyao ni ngumu kujikomboa na kupata hata maisha mazuri baada ya kumaliza utumishi wao, nataka niseme tutajadiliana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi tuone uwezekano wa kuwapatia viwanja, wengine wanastaafu na umri mdogo halafu hana hata nyumba wala kiwanja, tutaangalia namna ya kuwapatia viwanja angalau wale wa vyeo fulani fulani,” Simbachawene.