Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania inatarajia kuadhimisha Siku ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSD22) ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi Desemba 2022.
TPSD22 imeandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na wadau muhimu wa sekta binafsi na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili kuenzi na kutambua mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa nchi.
Zaidi ya wajumbe 1,000 ambao ni viongozi wa kisekta, wakurugenzi watendaji na maafisa waandamizi wa serikali watakusanyika kujadili dhima kuu ya “Kuimarisha Ushindani wa Sekta Binafsi”.
“Lengo la tukio hili ni kutathmini mafanikio ya sekta binafsi katika kipindi cha 2021-2022, huku tukiangazia mazingira bora ya biashara na uwekezaji ambayo yamechochea ukuaji wa uchumi chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita,” Angelina Ngalula.
Ongezeko la biashara na majirani zetu Kenya kwa asilimia 95 kumechangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Mafanikio mengine muhimu ya sekta binafsi ni pamoja na ukuaji wa shughuli za uwekezaji, upanukaji wa wigo wa ajira, masuala ya kodi, na bidhaa za Tanzania kufikia masoko mapya.
Ngalula alibainisha kuwa maadhimisho hayo ya Siku ya Sekta Binafsi yatatumika kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo. “Tunatakiwa kuueleza ulimwengu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania,” Ngalula alisisitiza.
Mwenyekiti wa TPSF alisema, kilimo ni sekta yenye kuleta faida kubwa kwa watu wenye nia ya kuwekeza. “Hivi karibuni tumesaini mikataba muhimu ambayo imepelekea mazao kutoka Tanzania kuuzwa nchi za nje. Kwa mfano, China imeagiza zaidi ya tani 40,000 za maparachichi kutoka Tanzania. Tumeshuhudia makubaliano kama haya yakifanyika baina yetu na Afrika Kusini na India.”
Kupitia diplomasia ya uchumi, Ngalula alisema, fursa za uwekezaji kwenye sekta ya madini zinatangazwa nje ya nchi na matokeo yake sasa yanaonekana. Mwaka 2021, serikali ilisaini mikataba minne na makampuni ya uchimbaji madini yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 735, mikataba hii ni yenye thamani kubwa zaidi nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa TPSF, kiwango cha ukuaji wa uchumi baada ya janga la UVIKO-19 kinatakiwa kuendelea, akisema kuwa hivi sasa uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 5.1.
Sekta binanfsi imekuwa sehemu ya kutoa suluhisho kwa changamoto za uchumi kupita biashara ndogo na za kati ambazo ni chanzo cha kipato kwa familia na uchumi wa taifa.
“Familia nyingi Tanzania zinategemea biashara ndogo na za kati, kwa mujibu wa Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA) takribani asilimia 35 ya pato la taifa linatokana na kundi hili. Maongezi yetu ya Disemba yatajikita katika nafasi ya sekta binafsi kwenye kuisaidia nchi kufikia dira yake ya maendeleo,” Ngalula alifafanua.
“Tutatoa zawadi kwenye vipengele vifuatavyo: (i) vyama vya biashara vyenye michango maalum kwenye sekta (ii) kampuni yenye shughuli bora zaidi za kusaidia jamii (CSR) (iii) kampuni inayochipukia (Startup) yenye ubunifu zaidi (iv) kampuni bora katika utunzaji endelevu wa mazingira, na (v) taasisi za serikali zinazowezesha biashara,” Ngalula alisema.