Rais wa Tunisia Kais Saied amfukuza kazi Waziri wa Uchumi na Mipango siku ya Jumanne na kumteua Waziri wa Fedha kuwa mkuu wa muda wa wizara hiyo, ofisi ya rais wa Jamhuri ilitangaza bila kutoa maelezo yoyote.
Katika taarifa fupi iliyochapishwa kwenye ukurasa wake rasmi, Ofisi ya Rais ilisema kwamba Mkuu wa Nchi “ameamua kusitisha majukumu ya Waziri wa Uchumi na Mipango Samir Saïed”.
Waziri wa Fedha Sihem Boughdiri amekabidhiwa jukumu la “muda” la kuchukua nafasi yake, taarifa hiyo iliongeza, bila kutoa maelezo zaidi.
Uamuzi huu unakuja wakati nchi inapitia mzozo wa kiuchumi na kifedha ambao haujawahi kutokea. Mfumuko wa bei ulifikia 9.3% mwezi Agosti, na ukuaji katika robo ya pili haukuzidi 0.6%, kulingana na takwimu rasmi.
Ikiwa na deni sawa na karibu 80% ya Pato la Taifa, Tunisia inashiriki katika mazungumzo magumu na Shirika la Fedha la Kimataifa ili kupata mkopo mpya wa dola bilioni mbili kufidia nakisi ya bajeti yake.