Kikosi cha polisi cha taifa cha Tunisia kimesema, nchi hiyo imevunja mtandao wa kusafirisha binadamu ambao ulisafirisha wahamiaji wa Afrika kwa njia haramu kwenda Italia.
Kikosi hicho kimetoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii ikisema idara za usalama katika mkoa wa Sfax kusini mashariki mwa nchi hiyo zimevunja mtandao haramu unaofanya biashara ya magendo ya wahamiaji wa kigeni.
Mtandao huo ulikuwa unarahisisha usafirishaji wa watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kuingia ardhi ya Tunisia kupitia mpaka wa Algeria, na kuwapeleka Italia.
Taarifa pia imesema watu wanne, magari matatu na pesa nyingi taslimu zilikamatwa kwenye operesheni hiyo.