Ajali hiyo ilitokea muda mfupi baada ya saa sita usiku wakati treni inayounganisha Tunis na Gabès (kusini) ilipoacha njia ilipowasili katika mji wa Msaken, takriban kilomita 150 kutoka mji mkuu.
Dereva wa treni alifariki wakati treni hiyo ilipopinduka kwenye lango la kituo cha Msaken. Mabehewa matatu kisha yaliacha njia, na kusababisha kifo cha abiria mmoja na kuwajeruhi wengine 34, limesema shirika la reli la Tunisia (SNCFT), katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Majeruhi 28 ambao wamelazwa hospitalini, waliweza kuondoka kwenye kituo hicho baada ya kupata huduma muhimu. Wengine sita watafanyiwa uchunguzi wa ziada lakini hali yao sio mbaya, kulingana na chanzo hicho. “Uchunguzi umefunguliwa ili kufafanua mazingira na sababu za ajali hiyo na kufafanua majukumu,” iimeongeza SNCFT.
Ajali hii inatokea miezi 15 baada ya ajali nyingine ya treni mbili zilizogongana kusini mwa Tunis na kujeruhi watu mia moja mnamo mwezi Machi 2022.
Mnamo Machi 2022, takriban watu 65 walijeruhiwa katika mgongano kati ya treni mbili katika mji mkuu wa Tunisia.
Takriban watu watano waliuawa na zaidi ya 50 kujeruhiwa mwishoni mwa 2016 wakati treni ilipogonga basi la umma kabla ya alfajiri karibu na eneo la ajali ya Jumatatu.
Mnamo Juni 2015, Tunisia ilikumbwa na ajali mbaya zaidi ya reli katika historia yake ya hivi karibuni, ambapo watu 18 walifariki katika ajali ya treni iliyogongana na lori huko El Fahes, karibu kilomita sitini kusini mwa Tunis.