Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amewataka watu kuondokana na dhana kwamba Wawekezaji Tanzania ni wenye ngozi nyeupe pekee yao na kusema hata Watu weusi tena Watanzania wanafanya mambo makubwa na kwa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) za juzi asilimia 61 ya Wawekezaji Tanzania ni Wazawa.
“Tulipodesign hii ziara ilikuwa nikiwaomba tumalizie hapa ili muondoe dhana kwamba Wawekezaji Tanzania ni wenye ngozi nyeupe pekee yao, nilitaka mjionee kwamba hata wenzetu weusi Watanzania wapo na wanafanya mambo makubwa, na kwa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) za juzi asilimia 61 ya Wawekezaji Tanzania ni Wazawa, ni Watanzania”
“Kwahiyo dhana kwamba tukizungumzia Wawekezaji tunazungumzia Wazungu tu na Wachina na Wahindi sio kweli, Watanzania kwa sasa wamehamasika wanawekeza na wanashika uchumi katika Nchi yao tuwapongeze kwa niaba yao”
Mkumbo amesema hayo Mlandizi Mkoni Pwani wakati alipoiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria kwenye ziara ya kutembelea mradi unaojengwa eneo la ekari 1077 wa kongani ya kisasa ya viwanda (Modern Industrial Park) inayotarajia kuwa na viwanda 202, bandari kavu na vituo vya umeme ikiwemo kituo cha umeme wa megawati 54.