Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki hafla ya utiaji saini wa Mikataba Mahsusi 3 ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam leo tarehe 22 Oktoba, 2023 Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.
“Kila pale ambapo sekta binafsi inaweza kuweka fedha, serikali tusiweke fedha – [badala yake] tuitumie kwa maendeleo ya jamii. Waje wawekeze, tufanye nao biashara, wapate, tupate. Na yale mapato ya serikali tuyapeleke kwenye matumizi mengine zaidi. Mmesikia hapa tuna asilimia kubwa ya watu wetu ambao ni masikini, tutumie kuwanyanyua katika ngazi tofauti tofauti,” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr Samia Suluhu Hassan.
“Katika mzunguuko wote wa majadiliano, nilichobaini ni kwamba sote Watanzania tunakubaliana kuwa tunayo changamoto pale bandarini. Tunatofautiana tu juu ya namna ya kuzitatua. Wapo wanaoamini sisi wenyewe bila mbia tungeweza kuzitatua. Ni mawazo mazuri ya kimapinduzi, lakini yapo mbali na uhalisia. Na njia hiyo itatuchukua muda mrefu sana kufika. Wakati Dunia inakwenda mbio, sisi tutakua bado tunasota. Na isitoshe tulishajaribu lakini hatukufanikiwa. Kwa hiyo mikataba hii imezingatia maoni yote yaliyotolewa kwa mtu mmoja mmoja na kupitia makundi ya kijamii pamoja na sheria na taratibu zote za nchi yetu. Nataka niwahakikishie kuwa maslahi yote mapana ya nchi yamelindwa”. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr Samia Suluhu Hassan.
“Nataka niwahakikishie kuwa au niwape uhakika Watanzania wote kwamba maslahi mapana ya nchi yetu yamezingatiwa. Kwa mfano amesema hapa Mkurugenzi hakuna atakayepoyeza kazi. Awe mwajiriwa wa bandari au hata wanaofanya kazi zao bandarini. Hakuna atakayepoteza kazi. Kutakuwa tu na kufuata mfumo fulani katika kufanya kazi zetu ili viwango zile vikae sawa tuendane na Dunia. Kinachofanyika kama nilivyosema ni kuhakikisha bandari inaendeshwa katika viwango vinavyokubalika duniani, kukuza ufanisi na biashara na hatimae kukuza mapato ya nchi yetu,” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr Samia Suluhu Hassan.