Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha usalama wa nchi na mipaka yake dhidi ya majanga mbalimbali unaendelea kuimarishwa ili kujiandaa na kuwa na utayari wa kukabiliana na majanga, maafa na dharura yoyote.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Machi 14, 2024) wakati wa ufungaji wa mafuzo ya zoezi la utayari dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi Tanzania, katika viwanja vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bandarini jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa moja ya jitihada hizo ni pamoja na kukamilisha maandalizi ya nyaraka mbili muhimu za Mpango wa Kitaifa wa Maafa ya Kikemikali, Kibaiolojia, Kiradiolojia na Kinyukilia. (CBRN National Action Plan) na Mpango wa Kuitikia wakati wa Dharura za Kinyuklia na Kiradiolojia (Radiological and Nuclear Response Plan) ambazo alizizindua katika hafla hiyo.
“Kupitia nyaraka hizi, mmeweka mikakati ya pamoja ya kitaifa ya namna ya kukabiliana na kujikinga na majanga yatokanayo dharura za kikemikali, kibaiolojia, kiradiolojia na kinyuklia. Nimefurahi sana kusikia nyaraka hizo zimezingatia masuala muhimu ya kisera, uzoefu wa kukabiliana na majanga kitaifa na kimataifa pamoja na matakwa ya kisheria na itifaki za kimataifa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka wizara zote na taasisi zinazohusika na kutekeleza mipango hiyo kuitumia kikamilifu na zitoe ushirikiano kwa wote wanaohitaji kutekeleza miongozo hiyo “Miongozo hii isiwe ni nyaraka za makabatini tu bali iwe miongozo ya utekelezaji wa hatua thabiti za kuhakikisha tunajenga nchi imara na salama. ”
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mafuzo ya zoezi la utayari dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi yalilenga kuwapa washiriki maarifa na ujuzi wa kukabiliana na vitisho vya kikemikali, kiradiolojia, kinyuklia na kusaidia juhudi kujiandaa na kukabiliana na majanga hayo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.