Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania bara Tundu Lissu leo amewasilisha hotuba yake ya kuufunga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka 2022 ambapo amezungumzia vitu mbalimbali na hizi ni baadhi ya nukuu zake.
“Hatuna budi kufahamu na kusambaza taarifa za kila mtu aliyekamatwa au kushtakiwa au kufungwa kwa sababu ya msimamo wake wa kisiasa au kwa sababu ya kutoa maoni yasiyowafurahisha Watawala”
“Ni mapambano ya kudai haki tu, sio kutegemea huruma za Watesi wetu ndio yatakayotuokoa, kwahiyo ushauri wangu wa siku kama ya leo mwaka jana bado una nguvu, hatuna budi kushughulikia tatizo la Wafungwa wa kisiasa na wa maoni, wa sasa na wajao”
“Tuwasaidie kwa michango Mawakili wanaowatetea Mahakamani, tuwatembelee magerezani au kwenye mahabusu za polisi na tusaidie ndugu au familia zao, kwa vyovyote vile tusiwafanye wajisikie wapweke katika saa yao ya uhitaji”
“Tutengeneze orodha ya kila aliyekamatwa, kuwekwa mahabusu au magereza au kushtakiwa au kufungwa kwa sababu za kisiasa na kosa alilotuhumiwa nalo, tufanye kampeni na kupaza sauti, ndani na nje ya nchi yetu ili Wafungwa hawa wa kisiasa na wa maoni waachiliwe huru”
“Salamu hizi zina uzito wa kipekee mwaka huu kwa sababu miongoni mwa wanaomalizia mwaka huu na kuanza mwaka ujao wakiwa ndani ya kuta za magereza ya Watesi ni pamoja na Mwenyekiti wetu wa Chama, Freeman Mbowe na Walinzi wake watatu” ——— Tundu Lissu.