Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri Ardhini (Latra) imetangaza nauli mpya za teksi mtandao na pikipiki mtandao ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika siku kumi na Nne toka tarehe ya kutangazwa kwa taarifa hii.
Akitangaza nauli hizo leo January 3, 2023 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Latra Habibu Suluo amesema nauli za teksi mtandao zinazobeba abiria wanne nauli itakuwa Sh3,000 hadi 4,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kuna safari nyingine toka hapo nauli itaongezeka kwa Sh800 hadi 1,000 kwa kilomita moja na safari inapokutana na vikwazo kama foleni nauli ya ziada kwa dakika itaongezeka kwa Sh80 hadi Sh100.
Kwa upande wa magari yanayobeba abiria sita nauli elekezi ni Sh4,000 hadi Sh5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kutakuwa na safari ya ziada toka ya awali nauli itaongezeka kwa Sh1,000 hadi Sh1,200 kwa kilomita moja na vinapotokea vikwazo kama foleni nauli itaongezeka Sh80 hadi Sh150 kwa dakika.