Uchafuzi wa hewa husababisha vifo vya mapema vya zaidi ya watu 1,200 wenye umri wa chini ya 18 kote Ulaya na huongeza hatari ya magonjwa sugu baadaye maishani.
Katika taarifa iliyochapishwa leo Jumatatu, Shirika la Mazingira la Umoja wa Ulaya linasema licha ya maboresho ya hivi karibunii, kiwango cha vichafuzi vya hewa katika nchi nyingi za Ulaya kinasalia juu ya miongozo ya Shirika la Afya Duniani” (WHO), haswa katika maeneo ya Mashariki na Kati mwa Ulaya.
Ripoti hiyo imechapishwa baada ya utafiti katika zaidi ya nchi 30, zikiwemo wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya na haikuangazia mataifa makubwa ya viwanda kama vile Russia, Ukraine na Uingereza, na hivyo yamkini idadi ya vifo kwa bara hilo ikawa ni kubwa zaidi.
Shirika la Mazingira la Umoja wa Ulaya ilitangaza Novemba mwaka jana kuwa watu 238,000 walikufa mapema kwa sababu ya uchafuzi wa hewa mnamo 2020 katika Umoja wa Ulaya pamoja na Iceland, Liechtenstein, Norway, Uswizi na Uturuki.
Shirika hilo lilisema uchafuzi wa hewa husababisha zaidi ya vifo vya mapema 1,200 kwa mwaka kwa watu walio chini ya umri wa miaka 18 huko Ulaya na huongeza hatari ya magonjwa mengine sugu baadae mnamo 2021, asilimia 95 ya watu wa mijini walivuta hewa ambayo haikukidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani.
Kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya WHO, uchafuzi wa hewa husababisha vifo vya watu milioni saba duniani kote kila mwaka. Maelfu kadhaa ya vifo vinahusu watoto chini ya miaka 15.
Nchini Thailand pekee, ambako moshi wenye sumu umeenea maeneo mengi, maafisa wa afya walisema wiki iliyopita kuwa watu milioni 2.4 walikwenda kupata matibabu hospitalini kutokana na matatizo ya kiafya yanayohusishwa na uchafuzi wa hewa tangu mwanzoni mwa mwaka.
Chembe chembe ndogo, hasa kutoka kwa magari na lori, ambayo inaweza kupenya kwa ndani ya mapafu, inachukuliwa kuwa kichafuzi kibaya zaidi cha hewa, ikifuatiwa na dioksidi ya nitrojeni na ozoni.