Hesabu za kwanza katika vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa rais uliocheleweshwa nchini Senegal Jumapili zinaonyesha mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye akiongoza.
Wafuasi wake walianza kusherekea mitaani baada ya siku ya amani ya uchaguzi ambayo wengi wanatumaini utaleta mabadiliko.
Mamilioni ya watu walijitokeza kumchagua rais wa tano wa Senegal kufuatia miaka mitatu ya msukosuko wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa na ambao ulichochea maandamano mabaya dhidi ya serikali na kuhimiza uungwaji mkono kwa upinzani.
Wapiga kura walitakiwa kumchagua mmoja kati ya wagombea 19 kuchukua nafasi ya Rais Macky Sall, ambaye anaachia ngazi baada ya muhula wa pili uliokumbwa na machafuko kutokana na kumfungulia mashtaka kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko na hofu kwamba Sall alikuwa na lengo la kurefusha muhula wake baada ya kikomo cha mihula kilichowekwa ndani ya katiba.
Rais aliye madarakani hakuwa kwenye orodha ya wagombea kwa mara ya kwanza katika historia ya Senegal.