Rais mteule wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ametupilia mbali ripoti za baadhi ya waangalizi wa kimataifa waliopinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Mnangagwa alikuwa akitoa hotuba yake ya kusherehekea Ikulu Jumapili na kusema kwamba alishinda uchaguzi kwa haki na hatakengeushwa na maoni mengine.
Ameongeza kuwa, “Ninafahamu kuwa baadhi ya wajumbe wa waangalizi walivuka wajibu wao na kuanza kuhoji sheria iliyopitishwa na bunge letu. Ni maoni yangu kwamba kila nchi huru inapitisha sheria yake kupitia bunge lao na Zimbabwe pia ilifanya hivyo.” Aidha amesema hakusimamia uchaguzi bali alishiriki kama mshindani na kuongeza kuwa: “Nina furaha kwamba nilishinda uchaguzi.”
Mnangagwa aliwashukuru wananchi kumchagua tena kuhudumu kama Rais wa Zimbabwe.
“Kuna kazi kubwa zaidi ya kufanya. Kwa pamoja, kama watu wamoja tulioungana tutaendelea na msururu wa ustawi ulioshuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hakuna mtu na hakuna mahali patakapoachwa nyuma”.
Aidha ametoa wito wa kuwepo amani baada ya uchaguzi.
“Hadi sasa, tumewaaibisha maadui waliotamani kuona tukiwa tumegawanyika na katika machafuko. Tutabaki kuwa watu wa umoja, wapenda amani na wastahimilivu, kuanzia Zambezi hadi Limpopo, Plumtree hadi Mutare, tukiimba wimbo mmoja wa taifa kwa fahari, chini ya wimbo mmoja na bendera ya taifa.”