Uchaguzi wa urais nchini Iran utafanyika Juni 28, televisheni ya taifa iliripoti Jumatatu, Mei 20, kufuatia kifo cha Rais Ebrahim Raïssi na wasaidizi wake katika ajali ya helikopta.
“Kalenda ya uchaguzi imeidhinishwa katika mkutano wa wakuu wa mahakama, serikali na Bunge,” televisheni ya serikali imeripoti. “Kwa makubaliano ya Baraza la Walinzi, imeamuliwa kuwa uchaguzi wa 14 wa urais utafanyika Juni 28,” televisheni hiyo imesema.
Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na wengine kadhaa wamethibitishwa kufariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili kaskazini-magharibi mwa Iran, televisheni ya taifa imesema.
Majina ya baadhi ya waliofariki katika ajali hiyo ya helikopta kando na Rais wa Iran Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian sasa yametolewa.
Shirika la habari la serikali IRNAA linasema kwamba ndani ya ndege hiyo pia alikuwemo Ayatollah Mohammad Ali Al-e Hashem, imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, na Jenerali Malek Rahmati, gavana wa jimbo la Irani la Azerbajani Mashariki.