Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa, amepinga Jumapili hii, Agosti 27, 2023 ushindi wa rais anayemaliza muda wake Emmerson Mnangagwa uliotangazwa siku ya Jumamosi jioni, na kujitangazia ushindi, baada ya uchaguzi uliokumbwa na hitilafu nyingi, ambazio zilitiwa shaka.
“Tumeshinda uchaguzi huu. Sisi ndio viongozi. Tunashangaa hata Mnangagwa kutangazwa mshindi […]. Tuna matokeo halisi,” Nelson Chamisa, wakili na mchungaji mwenye umri wa miaka 45 ambaye anaongoza Muungano wa Wananchi kwa ajili ya Mabadiliko (CCC), amesema katika mkutano na wanahabari mjini Harare.
Wakati huo huo rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, amesifia ukomavu wa demokrasia wa nchi yake, baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais, ili kuongoza kwa muhula wa pili, uliofanyika siku ya Jumatano.
Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80, ambaye Tume ya Uchaguzi imemtangaza kwa kupata ushindi wa asilimia 52.6 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Nelson Chamisa, aliyepata asilimia 44, amesema uchaguzi huo umeonesha kuwa Zimbabwe imekomaa na ni nchi huru.
Hata hivyo, ushindi wa Mnangagwa umekataliwa na upinzani, huku waangalizi wa Kimataifa, wakisema uchaguzi huo haukufikia vigezo vya kikanda na Kimataifa vya demokrasia.