Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe jana aliokoa jahazi baada ya kutoa Sh. milioni 20 na kuwezesha kufanyika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi wa uliomweka madarakani Evans Aveva.
Hanspoppe alitoa fedha hizo ili kugharamia uchaguzi baada ya kampuni ya bia Tanzania (TBL), ambao ndio wadhamini wa klabu hiyo, walioahidi kugharamia mkutano huo kushindwa kufanya hivyo kwa wakati.
Habari za ndani zilidai kwamba, rais aliyemaliza muda wake, Ismail Aden Rage alitaka uchaguzi usifanyike kutokana na wadhamini kutotoa fedha hizo.
Hata hivyo, uchaguzi huo uliohudhuriwa na wanachama 2,501 ulifanyika kama ilivyotarajiwa huku Aveva akionekana kukosa upinzani kutokana na kuenguliwa na Kamati ya Uchaguzi kwa aliyekuwa mpinzani mkubwa, Michael Wambura.
Mpinzani aliyesalia wa Aveva, Andrew Tupa hana umaarufu wa kutosha katika klabu hiyo na hivyo kumuacha Aveva katika mbio zilizoonekana za “farasi mmoja”.
Nafasi ya makamu rais ilikwenda Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyemshinda Swedi Mkwabi na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’.Mkutano wa uchaguzi huo ulifunguliwa kwa dua maalum saa 4:49.
Wambura alikumbana na balaa jingine baada ya kuzuiwa kuingia katika mkutano huo.Wakati huo huo, wakati kocha mkuu wa klabu ya Simba, Zdravko Logarusic, akisema hajui atarejea lini nchini, Kamati ya Usajili iko katika hatua ya mwisho kumnasa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uganda, Hassan Waswa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam, Simba iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa Waswa ili kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ushambuliaji.
Chanzo kilisema kuwa leo baada ya uongozi mpya kuingia madarakani utafanya maamuzi ya mwisho ya kuona ni wachezaji wangapi watabaki kuichezea Simba katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu.
“Logarusic anatua keshokutwa (leo) na yeye ndiye ataamua lini mazoezi yaanze rasmi…sisi kazi yetu ya kuimarisha timu tumeifanya kikamilifu licha ya kukutana na changamoto iliyohusicha uchaguzi mkuu,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hanspoppe Zacharia.
Hata hivyo, Loga alisema jana kuwa hajui atakuja lini nchini kwani bado hajapata taarifa zozote kutoka kwa Hanspoppe, hivyo anasubiri taarifa hizo.
Logarusic ambaye mkataba wake wa awali wa miezi sita ulimalizika Mei 31 mwaka huu anatarajiwa kuendelea kuliongoza benchi la ufundi la Wekundu wa Msimbazi akisaidiwa na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Selemani Matola.
Simba ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya nne na kukosa tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mwaka wa pili mfululizo.
Source: Nipashe