Chuo kikuu cha Dar es Salaam kimeipongeza serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kutoa uhuru wa kujieleza hasa kwa kuwapatia nafasi vyama vya Upinzani kusema maoni yao na wananchi kupata nafasi kutazama bunge mubashara.
Pongezi hizo zimetolewa leo Novemba 7,2023 Jijini Dar es Salaam na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam- Utafiti, Prof. Nelson Boniface wakati wa Mkutano wenye lengo la kujadili Uhuru wa kitaaluma, demokrasia na maendeleo endelevu katika bara la Afrika ulioandaliwa na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kupitia Ndaki ya Sayansi ya Jamii kwa kushirikiana na Jumuiya inayohusika na masuala ya sayansi jamii katika bara la Afrika (Codesria).
“Sisi kama taasisi ya elimu ya juu hilo ndio lengo letu kubwa la kuhakisha watu wanaweza kuzungumzia mawazo yao vizuri bila kuharibu uhuru au Sheria za nchi”. Amesema Prof. Boniface.
Kwa Upande wake Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii Prof.Christine Noe amesema mijadala hiyo wanayoizungumzia ina mahusiano ya moja kwa moja na maendeleo ya jamii hivyo watakapofanya tathimini ya tafiti zao waje na hatua za kufanya,ambapo lengo ni kuwajulisha jamii ya wanazuoni ni namna taaluma zao zinaweza kuleta matokeo katika jamii,
“Tuna vyuo vingi vimekutana hapa wote hawa tunajadili jambo moja kwa namna gani tuanzishe mijadala yenye tija na tuweze kusaidia jamii, tuweze kusaidia serikali,tuweze kusaidia mambo ya kisiasa na kijamii kwa ujumla”. Amesema
Nae Mwanazuoni Prof. Issa Shivji ametoa wito wa kuendelea kuwepo kwa Uhuru wa kitaaluma kwa kupatiwa Uhuru wa kitaaluma kwa wanataaluma bila hofu na kuingiliwa ili kuwa na maendeleo.
” Katika miaka ya 1980 Hayati Sokoine alipokuwa akitoa hotuba chuoni hapa alisema “huwezi kuwa na maendeleo bila mijadala” pia sisi tulikuwa wa kwanza kuandika tamko hili la Uhuru wa kitaaluma na wajibu wa kitaaluma mwaka 1999″. Ameeleza Prof.Shivji
Mkutano huo utakuwa kwa siku tatu kuanzia Nov 7- hadi Nov 9,2023 ambapo kuna ushiriki wa vyuo vikuu mbalimbali nchini kama Chuo Kikuu Cha Ardhi,Chuo Kikuu Cha Dodoma,Chuo Kikuu Cha Muhimbili na vyuo vya nje ya nchi kutoka Kenya, Rwanda, Burundi na Chuo kutoka South Afrika.