Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kimesaini mikataba ya ujenzi wa majengo 21 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yatakayojengwa Dar es Salaam, Lindi na Zanzibar kupitia mradi wa mageuzi ya kiuchumi katika elimu ya Juu (HEET).
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika leo Februari 2024 Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga ambaye amemuwakilisha Waziri Prof. Adolf Mkenda amesema kuanza kwa shughuli za ujenzi ni hatua kubwa na mafanikio ya kujivunia katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa elimu ya juu nchini na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Ni wazi kuwa kiasi cha fedha ambazo Chuo hiki kimetengewa si kidogo, hivyo Chuo kinatakiwa kuhakikisha kwamba ifikapo Juni 2026 fedha hizi ziwe zimeshatumika kutekeleza malengo ya Mradi”. Amesema Mhe. Kipanga.
Amesema kuwa Wizara itaendela kuratibu, kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo. “Tutaendelea kuwahimiza kuongeza kasi ya utekelezaji. Pale mtakapoona mnakwama kwa sababu yoyote ile muwe wepesi kuwasiliana na sisi ili tuona namna nzuri ya kukwamua mchakato”.
Aidha ameyataka makampuni yaliyosaini mikataba watambua kuwa ni wajibu wa kisheria na kimaadili wa kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa kadiri ya mkataba. “Tumesema kuwa fedha iliyotolewa kwa ajili ya kazi hii ni kubwa. Ni lazima thamani halisi ya fedha ionekane pale majengo yatakapokabidhiwa. Hili lijidhihirishe pia kwenye ubora wa majengo na kukamilisha ujenzi kwa wakati”.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amesema wamejipanga vizuri kuwasimamia wajenzi na wasimamizi wa ujenzi wahakikishe kuwa tunapata majengo bora na ya kisasa.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amesema Utekelezaji wa Mradi wa HEET umejikita kwenye kuimarisha na kuboresha miundombinu, ikiwemo ukarabati mkubwa na ujenzi wa majengo mapya pamoja na kufunga vifaa vipya kwenye majengo hayo.
Amesema Chuo kinajipanua na kuwafikia Watanzania zaidi kwa kuanzisha kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera katika fani za Kilimo na Biashara.
Hata hivyo amesema kuwa ili kuendana na matumizi ya TEHAMA, Chuo kimejipanga kuimarisha miundombinu ya TEHAMA ili kuboresha ufundishaji na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo ulinzi na usalama. Matumizi ya TEHAMA yatapewa msisitizo mkubwa kwenye kufundisha na kujifunza.
Meza kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali kwenye hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa majengo 21 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yatakayojengwa Dar es Salaam, Lindi na Zanzibar kupitia mradi wa mageuzi ya kiuchumi katika elimu ya Juu (HEET).