Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atazuru Tel Aviv Jumanne kukutana na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, Ikulu ya Élysée imetangaza hivi punde Jumapili usiku. Ziara ya mkuu wa nchi ya Ufaransa imekuja zaidi ya wiki mbili baada ya mashambulizi mabaya ya Hamas katika ardhi ya Israel, ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,400 wakiwemo raia 30 wa Ufaransa. Aidha, watu saba wa Ufaransa bado hawajapatikana.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atasafiri hadi Tel Aviv siku ya Jumanne kukutana na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, Ikulu ya Élysée imetangaza.
Kiongozi wa serikali ya Israel alitangaza muda mfupi kabla kwenye X (zamani ikiitwa Twitter) ziara inayokuja ya rais wa Ufaransa pamoja na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte.
Rais wa Marekani Joe Biden, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak tayari wamezuru Israel, kama alivyofanya mkuu wa serikali ya Italia Giorgia Meloni siku ya Jumamosi.
Emmanuel Macron kwa upande wake alisema akirejelea kauli yake siku ya Ijumaa kwamba atazuru Mashariki ya Kati ikiwa ataweza “kupata mambo muhimu” kwa ajili ya kanda hiyo kutokana na ziara hii.
Kisha akataja, miongoni mwa mambo hayo, “usalama wa Israel”, “mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi”, kusitishwa kwa mgogoro na kuanza tena “mchakato wa kisiasa” kuelekea suluhisho la serikali mbili, Israeli na Palestina.