Ufaransa itatenga euro milioni 80 za ziada kwa msaada wa kibinadamu kwa watu wa Palestina mwaka huu, na kufikisha jumla ya Euro milioni 100, Rais Emmanuel Macron alitangaza Alhamisi.
Rais wa Ufaransa alikuwa akizungumza wakati wa kuanza kwa mkutano wa kimataifa wa misaada kuhusu Gaza mjini Paris, unaoleta pamoja zaidi ya mataifa 50 kushughulikia mahitaji yanayoongezeka ya eneo la Palestina linalozingirwa ikiwa ni pamoja na chakula, maji, vifaa vya afya, umeme na mafuta.
Macron alitoa wito kwa Israel kuwalinda raia, akisema kwamba “maisha yote yana thamani sawa” na kwamba kupambana na ugaidi “hakuwezi kamwe kufanywa bila sheria.”
Alitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ya kibinadamu ili kuruhusu misaada kuwafikia raia wa Gaza.
“Tangu tarehe 7 Oktoba, Ufaransa imetangaza nyongeza ya Euro milioni 20 katika msaada wa kibinadamu na tutaongeza juhudi hii hadi Euro milioni 100 kwa 2023,” Macron alisema.
“Leo, pia natoa wito kwa nchi zote zilizopo kuongeza michango yao ya kifedha kwa raia wa Palestina kupitia Umoja wa Mataifa,” Macron alisema.
Alibainisha kuwa Umoja wa Mataifa unakadiria watu wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wanahitaji dola bilioni 1.2 (€1.12 bilioni) za msaada wa kibinadamu.