Mahakama nchini Uganda imewahukumu zaidi ya wanawake 100 kifungo cha mwezi mmoja kila mmoja kufanya huduma za jamii baada ya kukiri kuwatuma watoto wao kuomba omba katika mji mkuu wa Kampala.
Mahakama pia imepiga marufuku wanawake hao kurejea mjini na kuamuru warudishwe katika wilaya yao ya Napak kaskazini mwa Uganda, gazeti la kibinafsi la Daily Monitor liliripoti.
Wanawake hao waliomba kuhurumiwa, huku wengine wakisema ni wajane na wengine ni mama wasio na wenza, gazeti la serikali la New Vision liliripoti.
“Nimesikiliza kilio chao na hukumu [jela] haitakuwa sawa. Ni lazima nitekeleze adhabu ya kuzuia… nitawahukumu kufanya kazi za kijamii. Bila malipo, utatumikia kifungo cha mwezi mmoja,” hakimu katika mahakama hiyo Edgar Karakire, alinukuliwa akisema na Daily Monitor.
Kutuma watoto kuomba au kuomba msaada ni kinyume na sheria za ulinzi wa watoto za Uganda na adhabu yake ni ya juu zaidi ya miezi sita.
Wanawake hao walikuwa wamekamatwa mwezi uliopita wakati wa msako mkali wa kuwaondoa ombaomba kutoka mji mkuu, kabla ya mikutano mitatu ya kimataifa ambayo iliandaliwa huko.
Watoto hao walipelekwa katika Kijiji cha Watoto cha Masulita katikati mwa Uganda, ambacho ni mwenyeji wa watoto waliookolewa.
Article share tools