Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, amelaani hatua ya serikali kupitia jeshi la polisi kupiga marufuku mikutano ya hadhara ambayo amekuwa akiendeleza katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Polisi wanadai kuwa Bobi Wine amekuwa akitumia mikutano hiyo kumchafulia jina rais Yoweri Museveni na kukiuka utaratibu wa kuandaa mikutano hiyo.
Idara ya polisi imetangaza kusimamishwa mara moja kwa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji inayoongozwa na chama kikuu cha upinzani nchini Uganda chake Kyagulanyi, kutokana na kile wanachotaja kama ukiukwaji wa utaratibu wa umma na kashfa dhidi ya rais Yoweri Museveni
Msemaji wa polisi wa Uganda Fred Enanga, amesema shughuli hizi zimesitishwa hadi pale watakapofuata miongozo
‘Shughuli za uhamasishaji zimetumika kuchochea ghasia na kukuza ubaguzi wa kabila, kutoa wito usio halali wa kuondoa Serikali iliyochaguliwa ya jamhuri ya Uganda madarakani na kutoa kauli za kashfa dhidi ya mheshimiwa rais’.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, Bobi Wine alianza kufungua ofisi za chama katika maeneo tofauti ya nchi na pia amekuwa akifanya mikutano ya hadhara akiambia wanainchi ya kwamba kuna mpango wa kumuondoa madarakani rais Museveni na lengo la kuboresha hali ya maisha nchini Uganda.