Uganda imesema vifo vinavyosababishwa na UKIMWI nchini humo vimepungua kutoka 56,000 mwaka 2010 hadi 17,000 mwaka jana, ikiwa ni sawa na asilimia 70 katika miaka 12.
Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Uganda Daniel Byamukama amesema, katika mwongo mmoja uliopita, nchi hiyo imepata mafanikio makubwa katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI, na pia kupunguza vifo vinavyosababisha na virusi hivyo.
Ameongeza kuwa, mwaka jana, nchi hiyo ilikuwa na maambukizi mapya 52,000 ya VVU na watu 17,000 kufariki kutokana na ugonjwa huo, ikilinganishwa na mwaka 2010 ambao nchi hiyo iliandikisha maambukizi mapya 94,000 na vifo 56,000 vilivyotokana na UKIMWI.