Serikali ya Uganda Jumatano ilitangaza kuwasamehe waasi wa kundi la ADF endapo wataacha shughuli za uasi dhidi ya serikali.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa serikali ya Uganda ambaye pia ni waziri wa teknolojia ya habari na mawasiliano wa nchi hiyo Chris Baryomunsi, ambapo ameongeza kuwa serikali ya Uganda imetoa nafasi ya kuwasamehe wale walioandikishwa na kundi la ADF na kutaka kujisalimisha na kuacha mapambano dhidi ya watu wa Uganda wasio na hatia.
Wakiomba kusahemewa na kujitoa kwenye kundi la ADF, watasahemewa kwa mujibu wa sheria. Lakini hakueleza ni wakati gani.
“Tunataka kutangaza dirisha hilo la wao kuomba msamaha, kuachana na ADF, na kutoka nje. Watapewa msamaha kwa mujibu wa sheria,” Baryomunsi aliwaambia waandishi wa habari bila kutaja muda uliopangwa.
Takwimu kutoka kwa Tume ya Msamaha ya serikali ya Uganda zinaonyesha kuwa zaidi ya waasi 30,000 wa zamani ambao walichukua silaha dhidi ya serikali wamepewa msamaha tangu kuanzishwa kwa tume hiyo mwaka 2000.
“Iwapo hautapendezwa na hilo, basi unaweza kusubiri nguvu ya moto kutoka kwa UPDF (Vikosi vya Ulinzi vya Wananchi wa Uganda) na vikosi vya Uganda,” Baryomunsi aliongeza, akisisitiza kuwa msako wa kuwasaka waasi wa ADF unaendelea, na watafuatiliwa hadi wameshindwa, sawa na jinsi Lord’s Resistance Army wakiongozwa na Joseph Kony walivyoshindwa.