Serikali ya Uganda kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (UWA) imewahakikishia watalii usalama wao kufuatia shambulio la kigaidi la Jumanne jioni lililopelekea watalii wawili wa kigeni na mwongozaji wao mmoja raia wa Uganda kuuawa karibu na Mbuga ya Kitaifa ya magharibi mwa nchi hiyo.
Kwenye taarifa yake, Mamlaka ya Usimamiaji wa Wanyamapori nchini Uganda (UWA) imesema: “Watu wasiojulikana” walivamia gari la watalii hao na kulichoma moto kwenye eneo la Nyamunuka, kando ya Barabara ya Katwe inayoelekea kwenye mbuga hiyo ya taifa ya magharibi mwa Uganda.
Mamlaka hiyo imeongeza kuwa, inafanya kazi kwa bidii ili kubaini shambulio hilo limetokea katika mazingira gani na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kuwahakikishia watalii usalama wao.
Taarifa hiyo aidha imesema: “Usalama wa watalii wanaotembelea maeneo yetu ya hifadhi ni muhimu sana kwetu. Hifadhi zetu zote ziko wazi kwa ajili ya kupokea wageni, na tunaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kuhakikisha kuwa watu wote wanaotembelea hifadhi zetu wanakuwa salama.”